Juzi Jumapili 11.1.2015, maelfu ya waumini wa Kanisa la Full Gospel Bible Fellowship (FGBF) linaloongozwa na Askofu Mkuu Zachary Kakobe, walivaa TShirt zenye maandishi “UCHAGUZI USIFANYIKE JUMAPILI”, katika ibada maalum ya maombi kuhusu Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu. Katika maombi hayo maalum yaliyofanyika katika Kanisa hilo lililoko barabara ya Sam Nujoma, Mwenge, Dar-Es-Salaam; Askofu Kakobe aliwaongoza waumini hao kumshukuru Mungu kwa ajili ya roho ya usikivu iliyomwingia Rais Jakaya Mrisho Kikwete aliyetangaza katika hotuba yake ya Mwaka Mpya kwamba Kura ya Maoni kuhusu Katiba pendekezwa itafanyika ALHAMISI 30.4.2015. Katika maombi hayo, Askofu Kakobe alisema kwamba kwa miaka mingi, kilio cha Wakristo wengi kimekuwa kwamba siku ya kupiga kura isiwe siku ya Jumapili inayoingilia haki ya Kikatiba ya kupiga kura na uhuru wa kuabudu kwa Wakristo usiotakiwa kuingiliwa na mamlaka ya nchi, kama inavyoainishwa katika Katiba, Ibara ya 5 (1) na Ibara ya 19 (2); hivyo hawana budi kumshukuru Mungu kwa jinsi ambavyo Serikali ilivyosikia kilio chao, kwa kutangaza kwamba Kura ya maoni itafanyika Siku ya Alhamisi, badala ya siku iliyozoeleka ya Jumapili. Kwa msingi huohuo, waumini hao walimwomba Mungu katika maombi hayo kwamba, Serikali izidi kuwa na usikivu na hivyo kutangaza siku ya Uchaguzi Mkuu wa mwaka huu ambayo haitakuwa Jumapili, wala Jumamosi wala Ijumaa; ambazo ni siku za kuabudu kwa waumini wa madhehebu yote ya Wakristo, Wasabato na Waislamu; ili Wakristo na Watanzania wote kwa ujumla wapate kujitokeza kwa wingi kutumia haki yao ya kikatiba ya kupiga kura. Askofu Kakobe alisema kwamba imekuwa kawaida kwa wanasiasa kujiuliza kwa nini watu wengi hawajitokezi siku ya kupiga kura, bila kuwaza juu ya kujenga mazingira ya kuwawezesha watu wote kupiga kura, kwa kuifanya siku ya kura kutokuwa siku ya Ibada. Askofu Kakobe alitoa mifano ya nchi zinazotuzunguka ambazo hufanya Uchaguzi wao Mkuu kuwa siku ambayo siyo siku ya Ijumaa, Jumamosi au Jumapili; ili watu wengi wajitokeze kupiga kura, kwa mfano Zambia ambayo itakuwa na Uchaguzi siku ya JUMANNE 20.1.2015, baada ya Rais wao aliyechaguliwa katika Uchaguzi Mkuu wa JUMANNE 20.9.2011, kufariki. Vilevile alitaja siku za Uchaguzi Mkuu uliopita wa nchi nyingine kama ifuatavyo: Malawi (JUMANNE 20.5.2014); Zimbabwe (JUMATANO 31.7.2013); Kenya (JUMATATU 4.3.2013); Uganda (JUMATATU 18.2.2011); Rwanda (JUMATATU 9.8.2010); Burundi (JUMATATU 28.6.2010); na Afrika Kusini (JUMATANO 7.5.2014); na baada ya kutaja mifano hiyo, aliwaongoza waumini kumwomba Mungu ili kwamba Serikali iwe na usikivu katika jambo hili pia, na kutangaza Siku ya Uchaguzi Mkuu wa Mwaka huu wa 2015 katika nchi yetu Tanzania, kuwa siku yoyote ambayo siyo Jumapili, Jumamosi, wala Ijumaa; na kuifanya siku hiyo kuwa siku ya mapumziko maalum yenye kazi moja tu kuu, ya kupiga kura.
No comments:
Post a Comment