Ukitulia kidogo na kutafakari mstari huu nilionukuu, unaweza kuona kwamba maneno haya yanatufundisha kitu kikumbwa; Kwamba “mashtaka” asili yake ni uovu—ni ya kishetani! Sina shaka kwamba kila mmoja wetu amekuwa akikutana na matukio ya kushitakiwa mbele za Mungu. Usiniambie kwamba wewe umekuwa ukiishi katika mbingu za juu sana kiasi kwamba hujapata kushitakiwa na ibilisi!
Huyu mwovu hunena kupitia nia ya mwili na kutushitaki. Kadhalika kazi hii pia hufanywa na watumishi wake. Mojawapo ya ushindi ambao wana wa Mungu wanautazamia ni pamoja na kumshinda huyu “mshitaki.” Asifiwe Mungu kwa sababu maandiko yanaonesha kwa uwazi kwamba wakati ibilisi anafanya kazi ya kupeleka “mashitaka” kinyume na sisi, Mwokozi wetu Kristo Yesu anafanya kazi ya “maombezi” kwa ajili yetu.
Hata hivyo, ninafahamu kwamba ukweli mkuu unaohusu maombezi ya Kristo kwetu umefunikwa na theolojia ya wanadamu iliyochakachuliwa vibaya. Nina hakika ndugu yangu kwamba hata wewe umesikia kama mimi wahubiri wakijaribu kueleza huduma ya Yesu ya maobezi kwa watakatifu inavyofanywa, pamoja na mashitaka ya ibilisi kwetu. Melezo yao mengi ukiyasikiliza yanavunja moyo. Karibu wote (au wengi) maelezo yao yanafana na haya yafuatayo:
“Shetani ni adui na mshitaki wa ndugu zetu, husimama mbele za Mungu Baba huko mbinguni na kupeleka mashitaka ya wakristo mchana na usiku. Shetani humwambia Mungu madhaifu yetu yote, kushindwa kwetu kwote, huorodhesha dhambi zetu zote tuzifanyazo kwa mawazo, maneno na matendo na kumpelekea Mungu baba. Hutushitakia udhaifu wetu huo bila kusita, bila kukoma na bila huruma mbele za Baba.
Kwa upande wa Baba, yeye hudhihirishwa kama mwenye kukwazwa na kuchukizwa sana na dhambi zetu, na kwamba ana hasira na wale watendao dhambi; kwamba yeye yuko tayari kutoa adhabu kwa kusudi la kutuliza hasira zake. Hulazimishwa kufanya hivyo na asili yake ya utakatifu na haki ambavyo humfanya asipuuzie hata kijikosa kidogo bali kila kosa alipatie adhabu inayostahili.
Kutokana na upotofu huu wazazi wengi kwa kutojua wamepofusha mioyo na akili za watoto wao kwa vitisho hivi kwamba Mungu atawaadhibu vikali wakikosea na kwamba kila sekunde anawatazama ili wakikosea waadhibiwe ipasavyo. Hata mambo magumu zaidi wanaambiwa watoto wadogo kuhusu “ukatili” wa Mungu wao. Hili linamfanya Mungu aonekane kama mzee mkali, katili, mwenye kutoa adhabu kwa kusudi la kutuliza hasira zake, mwenye macho kama x-ray ambayo yanaweza kupenya sehemu yoyote hadi ndani ya mioyo ya wanadamu, na katika giza nene la usiku, huku akiwa ameshikilia bakora ya kutisha na kuwatazama kwa uso wa ukali!
Kuhusu Yesu, wahubiri wetu katika “video” hii humwonyesha kama mtu anayesimama mbele za Baba mwenye hasira kali, na kuomba kwa kubembeleza sana ili kutuliza hasira zake asiwapatilize wanadamu maovu yao kwa sababu ya hasira yake kubwa dhidi ya dhambi. Wanadai kwamba hasira ya Baba inaweza kutulizwa na kuridhishwa, na adhabu kuondolewa kama kaka yetu mpendwa, Bwana na Mwokozi wetu, Mwana wa Mungu wa kwanza, Yesu Kristo, mtetezi wetu, mwanasheria (advocate), atasimama kinyume na shetani mbele ya kiti cha hukumu cha Baba, na kumsihi Baba kwa niaba yetu, kwamba atusamehe kwa ajili yake tu, na kutuondolea adhabu kwa msingi kwamba yeye alikwishalipa gharama kwa ajili ya msamaha wetu. Kwa mujibu wa dhana hii hasira ya Mungu inaweza kutulizwa tu kama akikumbuka jasho la damu, mateso ya kikatili na kifo cha aibu alivyopata mwanae wa kwanza, Yesu.
Kwa maelezo hayo mafupi ndugu yangu, nashindwa kujizuia, na kwa hiyo sisiti hata kidogo kukuambia kwamba mafundisho ya jinsi hiyo si tu kwamba ni uongo uliopitiliza, bali pia ni upuuzi, ni takataka! Chimbuko lake ni kwenye mapokeo ya kirumi yanayomfananisha Mungu kama mtawala wa kiimla (dictator) katili, mwenye kuogofya, aliyekwazika, anayeridhishwa na kumwagika kwa damu za wale waliomkosea; na hili linamfanya Kristo awe kama mtetezi wa mtuhumiwa hadi kiongozi katili (Mungu) anaporidhika na hasira zake kutulizwa.
Si hivyo tu, bali pia inamaanisha kwamba kama asingekuwapo mtetezi wetu Yesu, Mungu angemsikiliza shetani katika yale mashitaka yake na bila kusita atuangamize au kutuadhibu vikali. Kwamba tungeweza hata kupoteza wokovu wetu na kutupwa jehanamu ya moto kwa sababu ya mashitaka ya shetani, kama mtetezi wetu mwenye rehema, Yesu, asingeingilia kati kila mara kumzuia Mungu, huku akimshawishi kwa kumwonyesha damu iliyomwagika kwa niaba yetu.
Huo ni uharibifu mkubwa wa kweli iliyo katika maandiko. Zaidi ya hayo, ni upuuzi wa kipumbavu na makufuru yasiyotamkika! Bwana asifiwe kwa sababu Roho wa kweli anazidi kuifunua kweli katika viwango vinavyoongezeka kila siku, na kwa njia hiyo tunauona utukufu wa Mungu ukizidi kuongezeka na asili yake ya upendo na rehema, hekima na nguvu, wema na fadhili ikizidi kufunuliwa, pamoja na kupata picha kubwa ya kusudi lake la vizazi na vizazi alilonalo kwa wanadamu.
Ninashawishika kupita mashaka ya kibinadamu kwamba hata shetani mwenyewe si mpumbavu kiasi cha kuamini kwamba angeweza kumkaribia Baba yetu kwa mashitaka dhidi yetu tulio watoto wake na kufanikiwa kumshawishi atuhukumu kwa sababu ya kushindwa kwetu!
Napenda kila anayesoma hapa afahamu kwamba hakuna sehemu yoyote katika maandiko inayosema kwamba shetani huwashitaki watakatifu KWA Mungu! Yasemavyo maandiko ni hivi: “ametupwa chini mshitaki wa ndugu zetu, yeye awashitakiye M-B-E-L-E za Mungu wetu, mchana na usiku.” Ni jambo moja kushitakiwa mbele za Mungu, na ni jambo jingine kabisa kushitakiwa kwa Mungu. Linatakiwa lieleweke vema kabisa kwamba SHETANI HAWEZI KUTUSHITAKI KWA MUNGU. Yeye hutushitaki mbele za Mungu. Ndugu yangu, SI Mungu Baba, Mwenyezi, ambaye shetani anatafuta kumshawishi juu ya udhaifu wako na kutokustahili kwako! Ni wewe mwenyewe!!!
Shetani hana tatizo katika kuelewa mipaka ya uwezo wake katika suala zima la kumshawishi Mungu mweza yote, ajuaye yote, mwenye hekima yote nk, juu ya udhaifu wako na kutokustahili kwako. Lakini kama akiweza kukufanya uamini hivyo, kwamba wewe umeshindwa, huna tumaini, kwamba haiwezekani wewe kuufikia mwito mkuu wa Mungu katika Kristo Yesu, kwamba ni jambo lisilowezekana kwako kugeuzwa na kuichukua sura ya Mwana wa Mungu, au kuufikia uzima usio na kikomo katika Kristo; kwamba wewe ni mwenye dhambi, kwamba Mungu hakupendi; kisha akafanikiwa kukuacha katika hali ya kuhukumiwa na kukosa tumaini, basi mashitaka yake yatakuwa yametimiliza kusudi lake la kukuibia tumaini lote, imani, ujasiri, amani, furaha na ushindi! Kwa njia hii Kristo hawezi kuumbika ndani yako.
Mtu awaye yote asifikiri kwamba jambo hili la mashitaka linafanyika huko juu, angani! Si kwamba shetani amesimama akiwa amevalia suti yake nyekundu mbele ya sofa kubwa jeupe halisi liitwalo kiti cha enzi na kutushitaki. Badala yake anazurura kwenye uharibifu na kutokuamini vilivyo katika nia zetu za mwili, katika sauti zisizokoma za dhamiri zetu zilizoharibika, katika fikra zilizopotoka na fahamu za kipuuzi juu ya Mungu..........SOMO LITAENDELEA HAPA HAPA KAARIBU............
No comments:
Post a Comment