Ufuatao ni ushuhuda wa Mwinjilisti Rodolfo kutoka Jamuhuri ya Domonika, ambao Bwana alimwonyesha kuhusiana na kuzimu, mbinguni pamoja na mambo yanayoendelea katika Kanisa la siku za leo.
Utangulizi
Mimi ni Mwinjilisti Rodolfo Acevedo Hernandez kutoka Jamuhuri ya Dominika. Koo langu limeathirika kutokana na usimuliaji wa ushuhuda huu lakini bado nitafanya hivyo tena leo hata kama kuna upinzani. Utukufu ni kwa Mungu! Tupo hapa kuhubiri Neno la Bwana Yesu Kristo na ninaenda kutoa ushuhuda ambao ulibadili maisha yangu na maisha ya maelfu kwa maelfu ya watu wengine!!
Hebu tuende kwenye Ufunuo 1:14-15: “Kichwa chake na nywele zake zilikuwa nyeupe kama sufu nyeupe, kama theluji; na macho yake kama mwali wa moto; na miguu yake kama shaba iliyosuguliwa sana, kana kwamba imesafishwa katika tanuru; na sauti yake kama sauti ya maji mengi.”
Kwa kuwa sikuridhika kuwa kwenye hali ileile ya kiroho niliyokuwa nayo, nilijifungia kanisani kwangu kwa siku nane; siku nane za kufunga na kuomba, nikiwa nimejifungia na Bwana Yesu. Kabla ya kuanza zile siku nane, Bwana, aliniambia hivi kupitia maono, “Rodolfo, ni wakati sasa ujiweke wakfu kwa ajili yangu,” na nilipewa vazi jeupe ambalo liliandikwa maneno: “Utakatifu kwa Yehova.” Baaya ya maono yale, mama mmoja mmisionari kutoka kwenye kanisa langu aliniambia, “Rodolfo, niliota kuwa Bwana ananiambia nikueleze kwamba: “jitenge na madhabahu (maana nilikuwa mhubiri); ninaenda kukuonyesha jambo kubwa ambalo litabadili maisha ya mataifa duniani.” Kwa hiyo, ndipo nikaanza mfungo wangu wa siku nane kwa Bwana.
Nilipata changamoto
Kwenye siku ya nne ya mfungo na maombi, nilikuwa nikiomba madhabahuni na ghafla, mbele yangu yalitokea mapepo mawili, ambayo niliyaona kama unavyoweza kumwona mtu uso kwa uso. Mapepo haya yaliniambia, “Rodolfo, hatutakubali wewe uvuke kizuizi chetu”, kisha mara moja yalitoweka. Nilianza kuwa na hofu kubwa maana unapoona viumbe wa rohoni kimwili, inaogopesha sana! Viumbe hawa walikuwa warefu na walikuwa na harufu ya salfa kama vile ndio wametoka moja kwa moja kwenye shimo la jehanamu. Walitumwa kuja kuniambia kuwa hawako tayari kuruhusu mimi nivuke kizingiti walichoweka. Lakini shetani ndiye pekee mwenye ukomo; Bwana Yesu Kristo alimshinda kwenye msalaba wa Kalvari. Utukufu kwa Mungu, haleluya!
Zilipopita siku saba, nilimwambia Bwana, “Bwana, siwezi kuendelea zaidi. Mwili wangu ni dhaifu. Sina nguvu za kutosha. Bwana, tafadhali nisaidie. Siwezi kutimiza jambo hili. Tafadhali, nisamehe; nipe nguvu.”
Ghafla, nilihisi mtu anatembea nyuma kuelekea kwangu, na akasema sikioni mwangu, “Rodolfo, usiache kuendelea na jambo hili hadi tukuonyeshe mambo ambayo uko karibu kuyaona.” Nilitiwa moyo na kujisikia ni mwenye nguvu zaidi. Siku iliyofuata, ilikuwa ni Jumapili. Nilijisikia dhaifu kidogo asubuhi. Jioni wakati wa ibada, kulikuwa na ujumbe wenye nguvu kutoka kwa Mwinjilisti Ruben Bells. Alipomaliza, nilikuwa nawasalimu ndugu zangu wote katika Kristo. Nilianza kuhisi kama pumzi zinaniishia. Nikawa nashindwa hata kupumua.
Ndugu wa kanisani wakanizunguka na kuanza kuomba. Ghafla, nilihisi kana kwamba kupitia kucha na vidole vyangu, kulikuwa na sindano zinapenya mwilini mwangu. Ubaridi wa zile sindano ulipenya mwilini kama hewa ya baridi na nikahisi pumzi yangu ya mwisho imeondoka na kwamba moyo wangu umesimama. Nilidondoka sakafuni na ndugu zangu wakaanza kujaribu kuniamsha. Walikuwa kama ndugu 12 hivi. Ghafla, nilihisi roho yangu ikitoka kwenye mwili na nikawa nautazama mwili wangu nikiwa nje, ukiwa umelala sakafuni. Hao wapendwa hawakujua kilichokuwa kikiendelea kuhusiana na mimi. Dada mmoja ambaye alikuwa ni nesi aliwaambia, “Amepata mshtuko wa moyo.” Nilikuwa natamani kwenda kwao na kurudi kwenye mwili wangu lakini nikawa nashindwa.
Kuzimu
Ghafla, nilihisi mwanga umepotea na nikaanza kupaa juu. Kule juu kuna mtu
alinisimamisha na nikaanza kushuka chini hadi nikafika mahali ambako nilihisi joto kali mno! Kisha, nikaona milango miwili myeusi inayonuka sana. Hapo ilikuwa ni kuzimu na kulikuwa kunatisha sana!
Nilipokuwa ndio niingie ndani ya ile milango, joka kubwa, ambalo kichwa chake kilijaa miiba na mwili wake ulifunikwa kwa nyembe badala ya magamba ya kawaida, lilitangulia kuingia kwenye gereza hilo. Nilipokuwa naingia kwenye milango ile, niliona macho ya kila aina ukutani, yakiwa yananiangalia. Lakini macho yale yalikuwa yamechorwa ukutani. Mara niliona macho mawili yananijia na kumbe lilikuwa ni pepo ambalo kifuani lilikuwa na bamba lililoandikwa: ‘Mimi ni Kisasi.’
Hukumu ya watumishi wasio waaminifu
Wakati huohuo, mapepo zaidi yalianza kutoka ukutani. Lile pepo linaloitwa Kisasi lilisema kwa sauti, “Mfalme Belzebub, tumempata mmojawapo aliye mkubwa ambaye aliendesha vita dhidi ya sisi, ufalme wa giza …” Biblia inasema: “Maana ingalikuwa heri kwao kama wasingaliijua njia ya haki, kuliko kuijua, kisha kuiacha ile amri takatifu waliyopewa.” (2 Petro 2:21). Kanisa linalomjua Bwana ni lazima liendelee kuwa thabiti na kutambua kuwa Yesu ndiye tumaini PEKEE kwa ajili ya wokovu wa roho zao.
Nikiwa ningali pale, lile pepo Kisasi lilikuja karibu yangu na kuniambia, “Rodolfo, nataka unitoe kama ambavyo ulifanya kule duniani.” Lilipokuwa likisema haya tena na tena, lilikuwa linaendelea kunitesa. Na nikaona mapepo mengi yamejipanga tayari kwa ajili ya kunitesa!
Mateso ya kuzimu kwa ajili ya wachungaji, wahubiri, na wainjilisti wanaoacha nguvu na upako wa Mungu ni makali zaidi kuliko yale ya roho zingine kule kuzimu! Uwe thabiti katika mwendo wako na Mungu! Hii ni saa ya Kanisa kuwa imara. Wakati ni sasa. Muda wa kuchezacheza kanisani umeshapita. Ni lazima tuwe na ujasiri na kuzishinda nguvu za kuzimu kwa jina la Yesu – Yeye peke yake ndiye nuru.
Mara kulitokea pepo lililoruka na kutupa mkuki kwangu ambao ulipita kwenye moyo wangu. Nilihisi maumivu yasiyoweza kuelezeka. Pia nilihisi kama vile kulikuwa kunanyesha salfa kule kuzimu. Nilihisi nyama ya mwili wangu inatoka kwenye mifupa na minyoo ikaanza kupekecha mifupa yangu.
Biblia inasema,“ambamo humo funza wao hafi, wala moto hauzimiki.” (Marko 9:48); na pia kwenye inasema, “Funza wametandazwa chini yako, na vidudu vinakufunika” (Isaya 14:11). Kuzimu ni mahali halisi. Yesu na Agano la Kale wanazungumzia kuhusu kuzimu.
Mara niliona kundi la mapepo wanaleta jeneza, lakini lilikuwa ni jeneza tofauti na haya tunayoyafahamu hapa duniani. Lile pepo Kisasi lilinishika sehemu ya chini ya mdomo wangu na kuniambia kwa dhihaka, “Rodolfo, nataka unitoe! Nguvu zako ziko wapi? Upako wako uko wapi? Uko wapi utukufu wako uliokuwa nao?”
Ujumbe ninaotaka uupate hapa ni kuwa, wakati mwingine kwa sababu tunahubiri, tunadhani kuwa upako ule ni wetu, na kwamba zile nguvu ni zetu, na kwamba uponyaji ni wetu. Biblia inasema kuwa utukufu unatoka kwa Mungu na utukufu ni wake pekee. Kwa sababu hiihii, ibilisi alitupwa nje ya Mbingu maana alitaka kutwaa utukufu wa Mungu. Kwa hiyo, wengi wanadhani kuwa wagonjwa wanaponywa kutokana na nguvu zao; na wenye mapepo wanafunguliwa kutokana na nguvu zao! Acha nikuambie kuwa, kile ambacho Bwana amekupa ni zawadi kutoka mbinguni. Ni rehema za Mungu kwa lengo la kuwafungua wanaoteswa, na pia ili roho ziweze kuokolewa.
Mimi ni ‘Niko’
Mapepo yalipokuwa yananiingiza kwenye lile jeneza, nilihisi upepo na kama kuna kitu kimedondoka sakafuni. Pepo Kisasi na mapepo mengine yalikimbia haraka na kujificha mbali na uwepo wake. Nilikuwa niko sakafuni kutokana na kuteswa na yale mapepo; na jambo la kwanza nililoona ambalo sitakaa nilisahau … Oh, Utukufu kwa Mungu! Niliona ‘mtu’ akiyejaa nuru … Haleluya!
Niliona makovu kwenye miguu yake. Nilipoinua kichwa changu, nilimwona huyu mtu wa ajabu, akiwa na mkanda kifuani mwake ulioandikwa: “Mimi ni MFALME WA WAFALME, na BWANA WA MABWANA.” Alikuwa amevaa taji kubwa sana la dhahabu kichwani mwake. Alinyoosha mkono wake kwangu na kusema, “Rodolfo, MIMI NI YESU na ninaenda kukuonyesha mambo mengi humu kuzimu, mbinguni pamoja na hali ya Kanisa langu duniani.” Alinishika mkono na kusema, “Twende sasa, Rodolfo.”
Ukahaba
Niliona amefungua chumba kikubwa ambamo kulikuwamo mwanamke. Akasema, “Naenda kukuonyesha adhabu ambayo shetani huwapa wale ambao walikuwa wakifanya ukahaba duniani. Kahaba anapokufa, anakuja kwenye sehemu hii. Angalia kwa makini, Rodolfo.” Niliangalia na kuona ndani ya chumba kile, mwanamke ambaye alikuwa amekaa mkao wa hatari sana, na nikaliona joka lilelile ambalo nililiona hapo mwanzo. Joka hili liliingia kwenye chumba kile kisha likajiingiza kwenye sehemu zake za siri. Kumbuka nilikuambia kwamba ngozi ya joka hili haina magamba ya kawaida bali ni nyembe.
Joka hilo lilipoingia, lilimharibu kabisa viungo vyake vya ndani, kisha likatokea mdomoni. Pepo linalosimamia ukahaba duniani linaitwa, “Metresa” au “Martha”, au “The Domineur”. Wakatoliki wengi wana “mtakatifu” huyu akiwa kama mwanamke ambaye mwili wake umeviringwa na nyoka; na pepo hili ndilo ambalo linawatesa makahaba kuzimu.
Bwana aliniambia kwamba ulikuwa ni wakati wa kuondoka hapo na tukamwacha mwanamke yule akilia kutokana na mateso na maumivu. Alikuwa akisema, “Nahitaji mtu wa kunisaidia!” Bwana akaniambia, “Rodolfo, hukumu imeshawekwa kwa ajili yao! Sasa Rodolfo, nitaenda kukuonyesha sehemu ambako shetani anawatesa wanawake ambao walitoa mimba za watoto wao duniani!”
Utoaji mimba
Ghafla, nilimwona mwanamke akiwa katika mkao wa kujifungua na nikaona pepo baya sana ambalo mikono na miguu yake ilikuwa kama ya farasi na mwonekano wake kama wa mnyama na alikuwa na keekee (drill) mikononi mwake. Keekee hii ilikuwa imejaa minyoo. Minyoo hii ilikuwa ni mikubwa sana na meno yao yalikuwa makali na miili yao ilijaa miiba iliyochongoka. Pepo lile liliingiza ile keekee kwenye sehemu zake za siri hadi akaonekana kama mwenye mimba.
Pepo lile likaanza kumpigia kelele, likimwambia kuwa azae huko kuzimu kwa kuwa alikataa kuzaa duniani. Kisha likasema, “Utukuzwe, utukuzwe shetani! Huu ni ufalme wako!”
Nilipomwuliza Bwana kwa nini adhabu ilikuwa kali kiasi kile kwa mwanamke yule, Bwana akasema, “Rodolfo, adhabu imeshawekwa kwa ajili ya mwanamke huyu!” Biblia inasema kwamba wauaji hawataingia kwenye Ufalme wa mbinguni. Watu wanatoa mimba au kuwaua watoto huku wakiamini kuwa huko ni kama kuua tu mnyama lakini kile hasa wanachofanya ni kuua mwanadamu mwenye roho na mwili.
Pepo lile liliendelea kumpazia sauti, likimwambia amtukuze shetani maana ule ulikuwa ni ufalme wake. Wale minyoo walianza kutoka kupitia tumboni mwa yule mwanamke huku wakiharibu kabisa sehemu za ndani ya mwili na kutoka wakiwa na vipande vya nyama midomoni mwao. Ungeweza kuona maumivu makali aliyokuwa akiyahisi. Bwana akaniambia, “Tuondoke kwenye sehemu hii.”
Shetani anashambulia watoto na familia
Tulienda kwenye sehemu iliyoonekana kama kuna fito nyeusi. Nikaanza kuona watoto wengi kule kuzimu. Nikamwuliza Bwana, “Kwa nini kuna watoto huku kuzimu?” Lakini Bwana akaniambia kuwa wale hawakuwa watoto; na kwamba ufalme wa mbinguni ni wa watoto na inabidi uzaliwe upya ili kuingia kwenye ufalme wa mbinguni.
“Sasa, Bwana vipi kuhusu watoto hawa?” niliuliza.
Bwana akaniambia tena, “Rodolfo, hawa si watoto”, kisha akaniambia nisikilize maagizo ambayo shetani alikuwa anawapatia.
Nilipogeuka, nikaona kuwa kumbe hawakuwa watoto bali ni mapepo na walikuwa wanacheza mchezo unaoitwaNintendo. Nikaanza kuona kila aina ya ‘programming’ na michezo ya kishetani, huku wakitoa alama na mijongeo kwa kutumia mikono yao, vyote vikiwa na makusudi ya kishetani.
Bwana alipowaamuru wageuke, ndipo nikaona jinsi sura zao zilivyo mbaya, za kutisha na zinazotia kinyaa. Shetani aliwapa maagizo akisema, “Wanangu, nendeni mkaue, mkaibe, na kuharibu.” Alikuwa yuko sahihi kwa sababu Biblia inasema kuwa shetani haji ila kuiba, kuchinja na kuharibu lakini Yesu alikuja ili kuleta uzima na uzima tele. (Yohana 10:10).
Wakati huo, hivi vipepo vidogo viliingia duniani na Bwana akaniambia kuwa hii ndiyo sababu watoto wa duniani wanajiua. Hivi sasa, wanasayansi na wanasaikolojia ya watoto hawaelewi ni kwa nini watoto wanajiua. Miezi michache iliyopita, mtoto wa kiume wa miaka 12 alimuua mama yake kwa kisu; mwingine alijinyonga hapa Marekani; na mtoto wa miaka 7 alimwua mama yake, wadogo zake na yeye mwenyewe kwa bastola ambayo aliipata. Mtoto mwingine alijitupa kutoka ghorofa ya pili na kufa. Barua wanazoacha hawa watoto zinasema kuwa maisha hayana maana pamoja na mambo mengine mengi.
Haya yanatokea kwa sababu mapepo yanaingia kwenye miili yao na kutawala fahamu zao na kuwafanya wachukue uamuzi wa kujiua. Iweni makini enyi wazazi na kile ambacho watoto wenu wanaangalia kwenye televisheni. Kile ambacho watoto wenu wanaangalia kwenye intaneti au wanachosikiliza kwenye redio kina athari kubwa. Mapepo yanaingia kupitia televisheni, redio, muziki na michezo ya vichekesho ya kishetani. Utukufu ni kwa Mungu, haleluya, kwa kutuamsha!!
Kisha Bwana akaniambia, ni kwa sababu hii ndoa nyingi zinaharibiwa, maana baadhi ya wazazi wanalaumu watoto wakidhani kuwa kwa sababu ya mtoto fulani, basi ni lazima wapeane talaka. Lakini mtoto si tatizo. Tatizo ni mashambulizi ya kipepo dhidi ya umoja wa ndoa na familia. Mwiteni Yesu Kristo! Liite Kanisa! Omba ufanyiwe maombi ili kuwa na nyumba isiyo na mashambulizi ya kipepo! “Sasa, Rodolfo,”Bwana akasema, “ni wakati wa kutoka wenye sehemu hii.”
Ibada ya sanamu
Tulipotoka kwenye sehemu ile, nilimwona mwanamke ambaye alikuwa amemezwa kabisa ndani ya moto. Mwanamke huyu alikuwa akilia sana akisema, “Kufa, kufa, kufa! Nitoe humu!”
Kile nilichoona ni kwamba, mwanamke huyu alishika mikononi mwake picha ya ‘Moyo mtakatifu wa Yesu’ kulingana na taratibu na mapokeo ya Kikatoliki.
Nikauliza, “Bwana, huyo ni mwanamke gani?”
Bwana akasema, “Rodolfo, mwanamke huyo ni bibi yako.” Biblia inasema kuwa waabudu sanamu hawataingia kwenye ufalme wa mbinguni (Gal. 5:20, Efe. 5:5). Bwana alinionyesha maisha ya bibi yangu yalivyokuwa duniani na nikaona kwamba kweli alikuwa ni mwabudu sanamu. Nikasema, “Bwana, tafadhali msaidie.”
Bwana akaniambia, “Rodolfo, sina cha kufanya! Hukumu imeshawekwa kwa ajili yake!” Kisha akaniambia, “Naenda kukuonyesha kile ambacho kitakuletea mateso duniani. Wengi hawataamini kile ambacho unaenda kukiona. Lakini usiwe na wasiwasi, nitakuwa pamoja na wewe.”
Celia Cruz (Malkia wa Salsa) yuko kuzimu
Mara nilimwona mwanamke ambaye miguu yake ilikuwa inapondwapondwa kwa visu ambavyo vilifika hata kwenye magoti yake kwa wakati uleule. Mwanamke huyu alikuwa akiteswa na mapepo mengi.
Bwana alinionyesha video ya Celia Cruz akifanya mikataba ya kishetani kule Hollywood kwa kutumia damu; na nikamwona akifanya mambo mengi ya kishetani. Bwana akasema,“Alikuwa ni mwabudu shetani. Alikuwa ni mfanya ibada ya sanamu. Alikuwa ni mchawi akiwa na maagano mengi ya damu. Kwa hiyo, muziki wake ulikuwa ukishika sana chati za juu. Ilikuwa ni vivyo hivyo kwa kundi lake la wanamuziki.” Na Bwana akanisikizisha muziki wake mmoja unaoitwa ‘Yemaya’, ambao ni maarufu sana kwenye ulimwengu wa Kihispania. Lakini unapoimba wimbo ule na kurudiarudia, maana yake hasa ni: ‘Mfalme shetani, njoo utawale ndani yangu!’ Na Bwana akaniambia, “Hukumu imeshapangwa kwa ajili ya Celia Cruz.”
Mwasisi wa Mashahidi wa Yehova yuko kuzimu
Tuliendelea kutembea na Bwana akanionyesha mwanamume mmoja mweupe ambaye mikono yake ilikuwa imetanuliwa. Na kitu cha ajabu kuhusiana na mtu huyu ni kuwa alikuwa na upanga mzuri sana ndani ya ulimi wake na upanga huu ulipenya hadi kichwani na kutokeza nje. Miguu yake ilikuwa imefungwa kwa minyororo na mgongo wake ulikuwa umejaa nyembe sehemu mbalimbali kwa namna kwamba, vyovyote ambavyo angejisogeza, ni lazima zinamkata. Nilipomwona mtu huyu katika hali hii, nikamwambia Yesu, “Bwana, tafadhali msaidie. Fanya kitu, Bwana Yesu. Hebu ona jinsi anavyoteseka kwa maumivu.” Bwana akaniambia, “Je, unajua huyu ni nani?”
“Hapana, Bwana,” nilisema. Niliona jinsi visu vilivyopenya kwenye ngozi yake na kisha kwenye mifupa na jinsi vilivyotokeza upande mwingine. Mtu huyo alipiga tu kelele kwa maumivu.
Bwana akaniambia, “Hukumu juu ya mtu huyu imeshatolewa. Sasa nitakuambia huyu ni nani.”
Kutokana na unabii huu, Bwana akasema,“Itakubidi kukimbia kutoka mji mmoja hadi mwingine maana jambo hili litakuletea mateso makubwa, lakini nitakuwa pamoja na wewe.” Akaendelea kusema, “Rodolfo, huyu mtu ni Charles T. Russell.” Nikasema, “Bwana, yeye ni nani?” Bwana akaniambia kwamba mwanamume yule alikuwa ni mwanzilishi wa kanisa la Mashahidi wa Yehova. Nikaomba, “Bwana, tafadhali msaidie,” na Bwana akasema, “Hapana, Rodolfo.”Kisha Bwana alifanya ishara kwa mkono, na mara moja nikaona roho nyingi zikiangukia kwenye shimo la kuzimu kwa kila namna. Walikuwa wakiangukia humo kichwa kwanza, miguu kwanza, tumbo kwanza, n.k.
“Rodolfo, kutokana na huyo mtu aliyelaaniwa, roho hizi zote zinaangukia kuzimu. Mtu huyu alifundisha kwamba Mungu ni Mungu wa upendo tu. Biblia inasema kwamba Mungu ni moto ulao. Mtu huyu, Charles Russell, aliondoa maneno ‘hell’ kutoka kwenye Biblia na akaondoa maneno yote ‘sheol’ na ‘Abaddon’. Pia, alikana uungu wa Yesu Kristo na pia alikana uungu wa Roho Mtakatifu, halafu akaweka tu neno Yehova kwenye Biblia. Aliondoa maneno Yesu na Roho Mtakatifu. Kutokana na mtu huyu aliyelaaniwa, roho hizi zote zinaangukia kuzimu.” (Ufu. 22:18-19). Kisha Bwana akasema: “Namlaani mtu huyu.”
Tafadhali enyi Mashahidi wa Yehova mnaonisikiliza wakati huu, si lengo langu kuwakwaza. Tokeni ndani ya kundi hilo na mje kwa Yesu haraka. Mimi siwachukii na wala sichukii dini yenu lakini mko ndani ya mahali pabaya. Njooni kwa Yesu. Anawangoja kwa mikono iliyo wazi kabisa. Charles Russell yuko kuzimu kwa sababu alifundisha uongo!! Msifuate uongo wake.
Tulipoondoka sehemu hii, milango hii ya gereza ilijifunga na moto ukawaka na mwanamume huyu, Charles Taze Russell, alipiga kelele na kumlaani Yesu tena na tena kwa sababu Yesu alisema, “Hukumu imeshaamuliwa kwa ajili ya mtu huyu.”
Kisha Bwana akasema, “Rodolfo, sasa nitakuonyesha magereza meusi ya kuzimu. Hii ni adhabu ya kupita kiasi ya shetani kwa roho zilizoko kuzimu.”
“Hapana, Bwana, tafadhali! Tayari nimeshaona mambo ya kutisha. Niondoe hapa, tafadhali …”
Bwana akasema, “Haya, Rodolfo, sitafanya kingine chochote kama hauniruhusu. Nitakupeleka mbinguni sasa.”
Mbinguni
Tuliondoka kwa kasi sana na tukafika mahali hapa. Malaika wawili walinisimamisha mbele ya milango hii iliyokuwa mizuri sana. Walikuwa wazuri
sana. Hawa malaika wawili waliniambia, “Rodolfo, ukiwa na mavazi hayo ya dhambi, huwezi kuingia kwenye ufalme wa Mungu.” Kwa hiyo, walinipatia mavazi mapya ambayo yameandikwa: Utakatifu.
Ujumbe sahihi
Wachungaji, wainjilisti, wahubiri na wamisionari, tafadhali samahanini na mnisikilize. Mungu hajawaita kuhubiri kuhusu utajiri au unabii juu ya hilo. Mungu amewaita kuhubiri kuhusu utakatifu na utakaso, maana bila utakatifu, hakuna atakayemwona Bwana. Pelekeni neno la utakatifu na kulihubiri!!!
Malaika waliniruhusu kuingia na Yesu alikuwa ananingoja na akaniambia, “Rodolfo mwanangu, karibu kwenye Ufalme wa Mungu wako.” Tulianza kutembea. Niliona kuwa barabara zilikuwa za dhahabu tupu, na nikaona mto uliokuwa kama kioo; ni maji halisi! Niliona pia almasi na mapambo kwenye mitaa, kitu ambacho watu wa duniani wanaweza kuuana kwa ajili yake! Kisha Bwana alinishika mkono na kuniambia, “Sasa nitaenda kukuonyesha hekalu.” Hekalu lilikuwa zuri sana! Niliona bilauri za dhahabu, vyombo vya dhahabu na nikasikia wimbo mzuri ambao ulikuwa unaimbwa na watoto. Bwana akaniambia kuwa waliokuwa wanaimba ni watoto ambao duniani watu waliwakataa lakini wana uzima kwenye ufalme wa mbinguni. Utukufu kwa Mungu, haleluya!
Mavazi ya harusi, chakula cha harusi, mataji
Tuliendelea kutembea mbinguni na nikaona mavazi meupe mazuri, yaliyopambwa kwa dhahabu pamoja na mataji juu yake. Bwana akaniambia lilikuwa ni Kanisa lake. Kwamba linatakiwa kuwa takatifu na lililotakaswa. Taji ni taji ya uzima na kwamba Bwana atakwenda kulipatia Kanisa.
Tulipotoka pale, niliona msururu mrefu wa watu waliovaa mavazi meupe. Niliona malaika wawili wakubwa, wenye sura nzuri ukiwatazama machoni. Niliona amani na upendo. Malaika mmoja akasema, “Karibu kwenye ufalme wa Mungu wako.” Malaika mwingine alipiga makofi. Niliona jinsi watu walivyo na furaha kuwa pale na sasa naelewa kile ambacho mtume Paulo alichosema kwamba, mateso ya dunia hii yanayopita si lolote ukilinganisha na utukufu unaotungojea kule mbinguni.
Bwana alinipeleka mahali ambako niliona meza ndefu sana isiyo na mwisho. Meza ilikuwa ya dhahabu. Kitambaa kilichoifunika kilikuwa cha dhahabu, bilauri za dhahabu, visu na nyuma za dhahabu, viti vya dhahabu, n.k. Kisha nikaona mataji makubwa kwa madogo na Bwana akaniambia kuwa yale mataji makubwa ni ya watumishi wake, pale watakapokuja kwenye harusi ya Mwanakondoo. Akasema, “Kwa vile harusi ya Mwanakondoo iko karibu kuanza, niko karibu kuja kuchukua Kanisa langu. Waambie kuwa ninakuja kulichukua Kanisa langu.”
Nikamwuliza Bwana, “Je, na haya mataji madogo ni ya nani?”
Akasema, “Hayo mataji madogo ni ya watu walio ndani ya Kanisa ambao wanaishi katika utakatifu lakini hawafanyi chochote kwa ajili ya Ufalme. Lakini nakwambia, usiridhike kupokea taji dogo bali fanya kazi kwa bidii kwa ajili ya taji kubwa. Fanya kazi kwa bidii kwa ajili ya Mungu ili aje kukupa thawabu ya uzima.”
Akasema, “Hayo mataji madogo ni ya watu walio ndani ya Kanisa ambao wanaishi katika utakatifu lakini hawafanyi chochote kwa ajili ya Ufalme. Lakini nakwambia, usiridhike kupokea taji dogo bali fanya kazi kwa bidii kwa ajili ya taji kubwa. Fanya kazi kwa bidii kwa ajili ya Mungu ili aje kukupa thawabu ya uzima.”
Jambo la ajabu lilikuwa kwamba, kila kiti kina jina nyuma yake na hakuna mtu mwingine yeyote ambaye atakikalia zaidi ya mwenye jina hilo!
Hali ya Kanisa la leo
Bwana aliniambia, “Sasa Rodolfo, naenda kukuonyesha hali halisi ya Kanisa ilivyo hivi sasa.” Nilimwona samaki mdogo akimsifu na kumwabudu Yesu kwa sababu Biblia inasema: Kila mwenye pumzi na amsifu Bwana! (Zab 150:6).
Kwa hiyo, Bwana alinionyesha dunia ambako ningerudi kwenda kuhubiri kile nilichokiona. Lakini nikawa na picha kwamba sikuwa na kumbukumbu kuhusiana na dunia na Bwana akanipa ufahamu kwamba, mtu anayeingia mbinguni, anasahau kila kitu kilichotokea duniani! Lakini sivyo ilivyo kuzimu. Kila anayeingia kuzimu, anakuwa na kumbukumbu za kila kitu alichotenda alipokuwa duniani, familia zao, na kwamba wasingependa waende kuzimu! Hayo nayo ni mateso mengine yanayoongezwa juu yao. Lakini yule anayeingia mbinguni, akili yake inabadilishwa ili ifanane na ufahamu wa kimbingu.
Bwana asifiwe! Kwa sababu hiyo, si Petro, wala Mariamu, wala Stephano, wala Elisha au Yohana mwenye kumbukumbu ya kile alichofanya alipokuwa duniani. Baada ya maisha yao ya duniani, wala hawana tena habari kamwe na kile kinachoendelea hapa. Petro wala hawezi hata kuwaza kuwa Kanisa Katoliki wanamwomba yeye au mtakatifu mwingine yeyote. Na Yesu akasema, “Hakuna jina jingine chini ya mbingu litupasalo kuokolewa kwalo.” Huyo ni Yesu Kristo, Mwana wa Mungu Aliye Hai. Na Mariamu alisema kule kwenye harusi ya Kana, “Lolote atakalowaambia, fanyeni.” Na … waabudu shetani wako Vatican. Wanaficha njia zote za dhambi za makasisi kutembea na watawa; makasisi kutuhumiwa kunajisi watoto na hata hapa kwenye Jamuhuri ya Dominika. Na Wakatoliki wanaendelea kuamini uongo huo. (Tafadhali ona pia ushuhuda mwingine wa ajabu: “Prepareto meet your God – Angelica Zambrano” Sehemu ya 1&2 ambao unaongelea zaidi kuhusiana na masuala ya Ukatoliki).
Watumishi wanaolenga fedha na wasio waaminifu
Sasa Bwana alianza kulia pale alipoanza kunionyesha mimi hali ya Kanisa. Ghafla, nilimwona mchungaji duniani amebeba begi kubwa lililojaa fedha. Bwana akaniambia, “Hawa ni wahubiri na wainjilisti wanaojitajirisha kutokana na matoleo kwa sababu wanafundisha uongo kwa watu wangu na kuwafanya watu wangu wapotee.”
Nawaambia enyi wahubiri na wainjilisti, mhubirini Yesu hata kama hakuna zaka au sadaka mnazopokea. Litakaseni Kanisa!
Mara niliona fedha za kwenye lile sanduku zimetoweka. Nilimwuliza Bwana naye akaniambia, “Kama ambavyo fedha zake zimetoweka, ndivyo na yeye atakayotoweka pamoja na mpinga Kristo. Lakini bado ninayo masalia ya watu wangu ambao hawajanajisika.”
Naona siku hizi jinsi wahubiri wengi, wachungaji, wainjilisti, n.k. walivyo matajiri na mamilionea. Hata hivyo, waumini wa makanisa yao wanaogelea kwenye umaskini, uhitaji wa chakula, huku mchungaji akiwa katika utajiri na wala hawasaidii! Wainjilisti wengi ni mamilionea wakubwa na hata mabilionea wakiwa na magari ya kifahari kupita kiasi. Je, Msamaria mwema yuko wapi?
Pia niliona wachungaji wengi wakihudumu kwenye madhabahu lakini nikamwona huyu mmoja akimalizia kuhudumu siku ile, akaondoka nyumbani alikokuwa mke wake, na kwenda kukutana na hawara yake ambaye anaishi naye pia; huku akiwa naye ni mshirika wa kanisa lake!
Nilimwona pia mwinjilisti akiondoka kanisani kwake na baada nyumba chache tu kutoka kwenye kanisa, akaenda kukutana na kahaba. Ni mwinjilisti yuleyule aliyekuwa akihudumu kwenye madhabahu! Bwana, tafadhali uturehemu!
Matendo yasiyo matakatifu – kujichua
Baada ya hapo, Bwana alinionyesha kundi la vijana wa Kanisa, kwamba wanapoondoka kanisani wanaenda kwenye sehemu ya giza maana wanadhani kuwa Bwana hawaoni. Wanapoenda huko wanaanza kujichua (kupiga punyeto) na kuzini dhidi ya miili yao wenyewe. Baada ya hapo, wanarudi na kuhudumu madhabahuni! Viongozi wa vijana, viongozi wa Kanisa! (Kama unahitaji msaada wa kushinda dhambi hii, angalia video hii).
Muziki usio na utakatifu kanisani
Sasa Bwana alinionyesha disko na Kanisa na akaniambia, “Angalia kwa makini.” Na mimi nikaangalia na kuona kwamba Kanisa lilikuwa ni sawasawa tu
na lile disko! Hakukuwa na tofauti yoyote! Walikuwa na mfumo uleule wa sauti, muziki uleule! Vifaa vilevile kutoka duniani vinaingia kanisani!
Dunia inatakiwa kubadilika iingie kwenye Ukristo lakini si Ukristo kuingia duniani! Tunaileta dunia kanisani! Pia niwaambie hili: Hatuwezi kumsifu na kumwabudu Mungu kwa kutumia Reggaeton, kwa Bachaton au Rock. Hata leo zipo nyimbo za Kikristo anazoimbiwa Mungu na pia zinaimbwa duniani kwa kutumia maneno yaleyale! Hazimtaji Mungu bali zinataja tu neno ‘upendo.’
Niliona pia muziki wa Rap na Perreo kanisani na hilo halikubaliki. Biblia inasema kuwa tunatakiwa kumwabudu Bwana katika uzuri na utakatifu (kwa ajili ya kuabudu kwa kweli, tazama Kol. 3:16 na Yoh. 4:23-24). Muziki wa Rock ni wa kishetani na ulibuniwa kuzimu.Wachungaji na wainjilisti, tafadhali, ondoeni makanisani muziki huo uliolaaniwa!!!
Bwana alinionyesha wanamuziki ambao wameshapotoka. Kwa upande mmoja wanaimba kanisani, na kwa upande wa pili wanaingia mikataba ya kuimba hata kwenye mahoteli kama waimbaji wa kujitegemea. Wanaenda kanisani kumsifu Bwana!
Ngoja niwaambie: muziki kama huo Bwana wala haukubali na tafadhali, samahani, ni lazima niwaambie ukweli - kile kinachotoka kwa Mungu ni kitakatifu na kimetengwa kwa ajili ya Mungu peke yake. Na kile ambacho wanamuziki wa leo wanakifanya, wanaenda kuimba kanisani, kisha wanapotea kutoka kwenye huduma, maana wanaonekana kama vile wanamwimbia Mungu kwa mkataba. Kwa hiyo, wanadhani hawana ulazima wa kuwapo pale muda wote wa huduma; wanaondoka mapema. Bwana aliniambia, “Kwa bahati mbaya, kanisa la aina hiyo halitaingia kwenye ufalme wa mbinguni.”
Masalia walio watakatifu
Baada ya hapo, Bwana alinionyesha kundi la watu – maelfu kwa melfu ya watu wanaojilinda katika utakatifu. Kwa mfano, nilimwona dada akimwambia mwingine, “Umekula leo? Nina kipande cha mkate nyumbani.” Nilimwona mwingine akiwa amebeba jozi ya viatu akimpelekea mwingine ambaye hana. Nikamwona mwingine akiwatia moyo wale wasio na nguvu. Wengine, kutokana na kujua matatizo ya wenzao, walikuwa wakiwasaidia na kuwaombea katika mahitaji yao bila mtu mwingine kujua.
Lakini leo, katika makanisa mengi, kuna masengenyo mengi kwa sababu watu hawajui kukaa kimya kuhusiana na watu wengine. Tubu leo! Yesu Kristo anataka kukupatia ukombozi na wokovu. Anaweza kukupatia zawadi ya toba.
Utukufu kwa Mungu!
Msifuni na kumwabudu Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana!
Msifuni na kumwabudu Mfalme wa wafalme na Bwana wa mabwana!
Rehema zake zadumu milele.
Mwinjilisti Rodolfo Acevedo
Chanzo: YESU NI NJIA BLOG
No comments:
Post a Comment