Vitendo vya kuvamiwa kwa makanisa nchini, vimekosa mwarobaini hivyo
kuvutia maadui wa ukristo kuendelea kuharibu nyumba za ibada bila hofu.
Tukio la hivi karibuni, Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG),
Mbezi Kati, kuvamiwa usiku tena wakati ambao vijana walikuwa wakiendela
na mkesha ni ushahidi kuwa hali inazidi kuwa mbaya badala ya suluhisho
kupatikana.
Mchungaji Samson Swai wa kanisa hilo, akizungumza na chazo cha habari
alisema kuwa, Ijumaa flani majira ya saa saba usiku, alipigiwa simu na
vijana waliokuwa katika mkesha kanisani hapo na kumjulisha kuwa palikuwa
na mtu aliyefahamika (jina tunalihifadhi kwa sasa) ameliharibu kanisa
kwa kubomoa milango yote.
Aliongeza kuwa mara baada ya taarifa hiyo alipiga simu kituo cha Polisi
Kawe, na kuwajulisha kuhusu tukio na walipofika eneo la tukio,mtuhumiwa
ambaye ni mkazi wa maeneo hayo alikwisha kimbilia nyumbani kwake.
Alisema, uharibifu uliofanywa na mtu huyo majira hayo ya usiku mnene bila sababu ya msingi ni kuing'oa milango vibaya.Kwa mujibu wa Mchungaji Swai, Polisi walionyeshwa nyumba anamoishi mtuhumiwa huyo na walipofika nyumbani kwake kwa lengo la kujua sababu ya kufanya uharifu huo, hakuwafungulia mlango licha ya kumgongea kwa muda mrefu lakini jitihada hizo ziligonga mwamba, hivyo Polisi kuahidi kumfuatilia.
Mchungaji Swai aliweka wazi kuwa, ikiwa Serikali haitaiangalia kati
suala la uvamizi wa makanisa na kulishughulikia kwa jicho pevu; huenda
vikatokea vita vya kidini, wakristo watakapochoka na matukio hayo kila
kona.
Mtumishi huyo alisema baada ya kushindwa kumpata mtu huyo, Polisi waliondoka eneo hilo, na kesho yake mtu huyo aliendelea kujigamba kuwa, Jeshi la Polisi limeshindwa kumtia hatiani ili aeleze nani anamtuma kufanya uhalifu katika nyumba ya Bwana.
Mtu huyo anayehisiwa kuwa, pengine alikuwa na silaha ya moto, anadaiwa
kuendelea kutamba mitaani kuwa hakuna wa kumfanyajambo lolote na
ataendelea na mashambulizi yake.
Pengine Serikali isipokuwa makini na kung'oa mizizi hii, hali ya vurugu
inaweza kuchukua nafasi mpya na kusababisha kutoweka kwa amani na
kuifanya Tanzania yenye sifa ya kuwa 'kisiwa cha amani' kupoteza sifa
hiyo ya kipekee na kuingia kwenye sintofahamu.
Chanzo chetu kilimtafuta Kamanda wa Polisi Mkoa wa kipolisi Kinondoni,
Camilius Wambura, ambaye alisema kuwa, taarifa ya kuvamiwa kwa kanisa
haijafika mezani kwake na kuahidi kulifuatilia, na kubainisha kibarua
hicho amemwachia OCD kulifuatilia kwa karibu ili apate taarifa.
Chanzo:Jesus vision
No comments:
Post a Comment