Saturday, November 23, 2013

USHITAKI WA SHETANI (PART TWO)

Na Fredrick Mulinda

..........Mtu awaye yote asifikiri kwamba jambo hili la mashitaka linafanyika huko juu, angani! Si kwamba shetani amesimama akiwa amevalia suti yake nyekundu mbele ya sofa kubwa jeupe halisi liitwalo kiti cha enzi na kutushitaki. Badala yake anazurura kwenye uharibifu na kutokuamini vilivyo katika nia zetu za mwili, katika sauti zisizokoma za dhamiri zetu zilizoharibika, katika fikra zilizopotoka na fahamu za kipuuzi juu ya Mungu.......... Endelea sasa

Sababu inayowafanya watakatifu wengi washindwe katika majaribu na mashitaka ya mwovu ni kwa sababu hawataki kumpinga shetani. Kwa miaka mingi tumekuwa tukifundishwa kumkimbia shetani, kujinasua katika miego yake, na tumekuwa tukifanya hivyo. Lakini katika siku hii ya kutiwa nuru ya kweli, wote walioangaziwa wamegundua kwamba ni joka yule yule, yule joka mkubwa, ambaye amekuwa akitutishia tumkimbie na kumwogopa badala ya kumpinga, na kwa sababu tumekuwa tukikimbia, amefanikiwa kwa kiasi kikubwa “kuponda visigino vyetu”; na la kusikitisha zaidi ni kwamba tumekuwa tukifanyiwa hivyo tukiwa ndani ya nyumba yetu! Pia ni joka yule yule ambaye amekuwa akitushitaki mchana na usiku mbele za Mungu katika hekalu lake ambalo ni wewe na mimi, na mbele za kiti cha enzi cha Mungu ambacho kiko ndani ya roho zetu!
Unaona! Maono ya joka aliyoyaona Yohana yanafunua asili/tabia ya joka la kiroho, lakini shetani haji katika mwili kama jitu lenye pembe, mkia na sura ya kutisha. Huja katika tamaa zako mwenyewe. Husema katika mawazo yako mwenyewe. Hukutesa kupitia hisia zako mwenyewe. Vita hufanyika katika mawazo yako mwenyewe akinena maneno ya mashitaka ndani yako mwenyewe. Huandaa kesi yako na kuisoma katika roho yako mwenyewe. Kadhalika Mungu naye yuko huko huko. Roho wa Mungu anayekaa ndani yako naye hunena kutokea huko huko ndani yako, katika nia yako ya roho, katika patakatifu pa patakatifu pa roho yako, akinena maneno ya faraja, tumaini, ushindi, neema nk.
Sauti ya Baba hutupa uhakika na neema kuu. Twamsikia akisema, “Nakupenda mwanangu; mimi nimekuzaa, na nitakuwa baba kwako; Nitakutia nguvu, nitakushika kwa mkono wangu wenye nguvu, maana mimi ni mwaminifu nami nitaitimiliza kazi niliyoianza ndani yako na kukuleta katika utukufu bila kunyanzi wala waa.”
Na hapo hapo, mbele za Mungu, katika hekalu lake—ndani—huibuka sauti ya upinzani, sauti ya nia ya mwili, nia ya kidini—mshitaki! Ni huko huko katika fikra, katika mbingu za ulimwengu huo ambao ni wewe, ambako shetani anatakiwa atolewe na kuangushwa, yeye pamoja na kila kitu kilichoinuka kijiinuayo juu ya elimu ya Mungu aliye ndani yako!
Kweli shetani anaweza kutushitaki, lakini Mungu hatatuhukumu. Shetani ni mshitaki/mwenye kuhukumu. Sasa, kama Mungu atatuhukumu basi atakuwa akifanya shughuli moja na shetani—watakuwa wabia! Lakini je, Mungu yuko upande wetu au kinyume chetu? Rumi 8:31-34 inaweza kutupa majibu. Lakini tunajua kwamba huyu baba yetu wa ajabu, Huyu mkombozi wetu, mwenye upendo kuliko viumbe vyote, ndiye aliyegeuza mioyo ya baadhi yetu na kuielekeza kwake. Mungu baba alimtuma Yesu afe msalabani ili atukomboe. Lakini bado dini inatuambia kwamba sharti Yesu atulize hasira zake kwanza. Lakini ukweli ni kwamba Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanae wa pekee, Yesu. Hatukumchagua sisi bali yeye ndiye alituchagua. Tunampenda kwa sababu alitangulia kutupenda. Sasa ni nani mwenye kuhukumu? Hakika si Mungu! Sasa basi hakuna hukumu ya adhabu kwao walio katika Kristo Yesu. Nini kitatutenga na upendo wa Mungu ulio katika Kristo Yesu? Jibu lake ni la hakika. Hakuna kiumbe chochote katika ulimwengu wote kinachoweza kututenganisha na upendo wa Mungu.
MAOMBEZI YA YESU
Ina maana gani hasa kusema kusema kwamba Yesu anatuombea/anatutetea?Ah! Kila nikisoma neno la Mungu na kujifunza kwa roho wake wa kweli mambo mengi yanakuwa wazi, na mojawapo ni kwamba, ijapokuwa maombezi ya Kristo kwetu yanamwelekea Mungu, maandiko yanadhihirisha kwamba “msukumo” wa kwanza wa maombezi hayo SI kumwelekea Mungu, bali kumwelekea mwanadamu, kuelekea upande wetu, kutusogeza kwa Mungu, kutuvuta kuelekea kwa Baba, kutenda kazi kwa nguvu ndani yetu, ili tuweze kujiachia kwake, kuuishi ufunuo wa roho yake katika maisha yetu.
Ni kweli Yesu ni mpatanishi wetu, mwombezi, mwanasheria (advocate), anasimama kati yetu na Mungu. Lakini nini hasa afanyacho? Je, ni kweli kwamba anatuombea kwa Baba ili aturehemu? Hapana! Hakuna kitu kama hicho! Neno la kiyunani litumikalo ni “entuchano” likiwa na maana ya “kukutana na, kuzungumza na, kusihi.” Sasa swali libaki kuwa hili: Ni yupi huyo ambaye Yesu anakutana naye, anazungumza naye au anamsihi? Ni Mungu au ni mwanadamu? Mungu aliupenda ulimwengu hata akamtoa mwanawe wa pekee kwa ajili yetu. Je, ndiye huyu huyu tena anayehitaji mtu akutane naye, azungumze naye au amsihi??? Je ni huyu Baba aliyeupenda ulimwengu anayehitaji mtu amsihi ili awe mwenye rehema na neema kwetu? Sikiliza! “yaani, Mungu alikuwa ndani ya Kristo, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho”
Kwa hiyo tunaona kwamba maombezi ya Yesu ni kutuelekea sisi (to us-ward), kukutana na sisi, kuzungumza na sisi, kutusihi sisi, kutupatanisha sisi, kuufunua moyo wa Baba kwetu, kuturejesha kwa Baba ili kwamba tupatanishwe nay eye! Shughuli yote ya maombezi ya Kristo imetuelekea sisi na si Mungu. Mungu hahitaji kupatanishwa na sisi. Ni huyo huyo Mungu asiyeonekana, asiyejulikana, aliyemtuma Kristo kwetu, kukutana nasi, kuzungumza nasi, kutuvuta sisi ili kwamba sisi na Baba tuwe umoja tena. Si jambo la kubariki moyo hilo?
Ni wakati wa kunasuka katika mitego ya huyu mwovu ambayo kwa hiyo wengi wametegwa (2Tim 2:26). Ni mashitaka makubwa kama nini na hukumu isiyotamkika ambavyo huyu joka ajifanyaye malaika wa nuru amekuwa akiwarushia ndugu zetu katika Kristo. Kati ya udanganyifu wake mkubwa uletao utumwa ni pamoja na kuwafunga watu katika kweli nusu—kuwaachia kweli inayotosha tu kuwaweka utumwani badala ya kweli yote inayoweka huru. Kuharibu kweli kwa kiwango ambacho wasikiaji hupata majibu yasiyo sahihi na kubaki na maswali yasiyojibiwa, na wakati mwingine kuogopa hata kujiuliza maswai hayo! Kila wiki Cathedro zinajaa wafungwa wa mshitaki wa ndugu zetu, na bado hawaielewi kweli ijapokuwa sauti za “manabii” zinapaa juu kama sauti ya tarumbeta huku maandiko mengi yakisomwa mbele zao kila sabato (Acts 13:27).
Ni ufunuo kamili tu unaoweza kufukuza uongo wa mshitaki wetu, na kadri tunavyoifahamu kweli ndivyo uwezekano wa kudanganywa unavyopungua. Tumepewa Roho Mtakatifu atuongoze katika kweli, si nusu, bali yote.
Mara zote ibilisi asipofanikisha kutudanganya kwa njia ya vitisho hujaribu njia hii ya mashitaka. Njia hizi mbili zinatoka ndani na nje. “Shetani wa dini zetu” hutuhukumu/hutushitaki kutokea kwenye fikra zetu wenyewe kutokana na kweli nusu nusu za kidini tulizomeza. Njia nyingine ya kutushitaki ni kuendelea kutuhubiria habari za dhambi zetu na upungufu wetu na kushindwa kwetu. Jambo hili lazima limfanye mtu ajihukumu, na kama tukiweza kujihukumu, hakutakuwa na hitaji la mwingine kutuhukumu; kwa maana mshitaki atakuwa amefanikisha utume wake.
Kadri unavyozidi kumfahamu Mungu, kujisogeza kwake, kufahamu kweli yake na kuisema bila hofu ndivyo mashitaka yanavyozidi kuwa mengi. Mojawapo ya sababu ya mashitaka kwa ndugu waliopiga hatua ya ukuaji ni kule kunasuka kwao katika kongwa la dini. Maneno ya watu walio huru huonekana kama vile yanatishia mamlaka za wakuu wa dini, yanatishia mfumo wa kanisa la kitaasisi, na hasahasa na vyanzo vya mapato na utajiri wa taasisi hizo. Ukisema kinyume na hayo ndipo utakapojua kwamba sehemu kubwa ya utendaji kazi wa shetani si katika baa, si katika danguro, si katika vijiwe vya bangi, au katika ulimwengu wa misukule—ni katika dini! Utashitakiwa kwamba tumepotoka kiimani, kwamba una mafundisho potofu, kwamba unakufuru na mengine mengi. Wakuu wa dini wataonesha kwa uwazi kabisa kwamba kama tusipoungana nao na kusema yale wanayosema siku zote, utakuwa umejitenga nao, umekataa kutii mamlaka iliyowekwa, na kwa sababu watakufukuza au wewe mwenyewe utaona mazingira yao hayakufai tena, basi utashutumiwa kwamba “umeacha kukusanyika kama ilivyo desturi ya wengine” (hahahaha!), umepoteza mwavuli wao, na bila wao huwezi kupata njia nyingine ya kuijua kweli!!!

 

No comments:

Post a Comment