Monday, August 4, 2014


Ufufuo na Uzima Kufanya Uzinduzi wa Mikutano yake ya Injili Nyanda za Juu Kusini



Na Mwandishi wetu. 


Sehemu ya Vyombo vya Muziki vitakavyotumika siku ya Uzinduzi
Kanisa la Glory of Christ Tanzania maarufu kama Ufufuo na Uzima linaloongozwa na Mchungaji Kiongozi Josephat Gwajima ambaye Mungu amempaka mafuta kufufua wafu na kurudisha misukule (watu waliokufa katika mazingira tata) linatarajia kufanya uzinduzi wa Mikutano yake ya Injili kesho Jumapili 3 Agosti 2014 kuanzia saa 3 asubuhi katika viwanja vya Tanganyika Packers kuelekea nyanda za juu kusini  na baadaye magharibi mpaka kaskazini mwa Tanzania baada ya kufanya mikutano kama hiyo Mashariki mwa Tanzania ikiwa ni pamoja na Arusha, Moshi, Tanga, Morogoro na Kilombero.


Itakumbukwa kuwa mwezi Septemba mwaka 2013 Ufufuo na Uzima ilianza rasmi mikutano yake ya injili ambayo kwa wastani zaidi ya watu milioni moja (1,000,000) walihudhuria mikutano hiyo iliyofanyika Arusha, Moshi, Tanga, Morogoro na Kilombero mpaka mwezi Disemba mwaka 2013.

Uzinduzi huo wa Mikutano ya Injili kuelekea nyanda za Juu kusini inatarajiwa kuanza mkoani Iringa mwishoni mwa mwezi Agosti, na kuelekea Njombe, Songea, Mbeya, Sumbawanga na Katavi. Ratiba kamili ya Mikutano hii inatarajiwa kutolewa kesho katika uzinduzi huo.


Uzinduzi huu utapambwa na shamra shamra za waimbaji maarufu wa nyimbo za Injili hapa nchini akiwemo Rose Mhando, John Lisu, Bonny Mwaitege, Ambwene Mwasongwe, Jackson Benty, Christina Shusho, Upendo Nkone na Flora Mbasha. Wengine ni pamoja na Munishi ambaye pia ameambatana na Malebo, aliyewahi kumtaja katika kibao chake maarufu cha Malebo hataki kuokoka.

Maelfu ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanatarajiwa kuhudhuria uzinduzi huu. Watu mashughuli mbalimbali pia wanatarajiwa kuwepo ikiwa ni pamoja na Mbunge wa jimbo la Kawe Mhe. Halima Mdee.

No comments:

Post a Comment