|
Askofu Zachary Kakobe. |
NENO LA MSINGI
YOHANA 16:24
“Hata sasa hamkuomba neno kwa jina langu: OMBENI, NANYI MTAPATA; furaha yenu iwe timilifu”.
Maneno haya aliyasema Yesu Kristo mwenyewe akiwaambia Wanafunzi wake. Tunaona katika maneno haya kwamba, kila mwanafunzi wa Yesu au mtu aliyeokoka, ana haki ya kumwomba Baba yetu aliye mbinguni kwa Jina la Yesu Kristo na akapokea jibu. Yesu hasemi kwamba mtu fulani tu aliyeokoka akiomba, ndiye atakayepata jibu, bali YEYOTE.
MARKO 11:23
“Amin, nawaambia, YEYOTE atakayeuambia mlima huu, ng’oka ukatupwe baharini, wala asione shaka moyoni mwake, ila aamini kwamba hayo asemayo yametukia, yatakuwa yake. Kwa sababu hiyo nawaambia, yoyote myaombayo mkisali, aminini ya kwamba mnayapokea, nayo yatakuwa yenu.”
Maandiko mengi yanadhihirisha jinsi ambavyo kila mtu aliyeokoka alivyo na haki ya kuomba na kupokea jibu na wala siyo mtu fulani pekee. [Angalia mifano katika YOHANA 14:12-14; MATHAYO 7:8-11].
ANGALIA TENA LUKA 11:10; “ Kwa kuwa KILA AOMBAYE HUPOKEA…….”.
Unaona! Kila mtoto wa Mungu, yaani kila mtu aliyeokoka, akiomba, hupokea. Huu ni UHONDO maalum kwa watoto wa Mungu tu. Mtu ambaye hajaokoka, ametenganishwa kabisa na Mungu kutokana na maovu yake. Kutokana na dhambi za mtu ambaye hajaokoka kumfarikisha au kumtenganisha na Mungu, sala zake ni machukizo mbele za Mungu na hazisikilizwi kabisa. [SOMA ISAYA 59:2; MITHALI 28:9; MITHALI 15:29; YOHANA 9:31]. Sala pekee ambayo inasikilizwa na Mungu inapotoka kwa mtu ambaye hajaokoka, ni pale anapotubu dhambi zake na kuwa tayari kuziacha na kuomba damu ya Yesu imsafishe uovu wake; ili aokolewe kutoka katika mauti ya milele [1 YOHANA 1:7-9]. Mtu ambaye hajaokoka, akimpokea Yesu Kristo kuwa Bwana au Mtawala wake na mwokozi wake ndipo anapofanyika MTOTO WA MUNGU na kuanza kufaidi uhondo wa kujibiwa maombi na Baba yetu aliye mbinguni [YOHANA 1:12]. Kabla ya kuokoka, mtu anakuwa ni mtoto wa Ibilisi, na siyo mtoto wa Mungu [YOHANA 8:44]. Kwa sababu hiyo ili uingie katika mpango wa Mungu wa kukupa majibu ya maombi, kwanza ni lazima ukubali kuokolewa na kuwa mtoto wake.
KUTEGEMEA KUOMBEWA NA MWINGINE WAKATI WOTE
Ni huzuni kwamba, wako watoto wa Mungu ambao wanafikiria kwamba wao hawawezi kusikilizwa na Mungu na kujibiwa; mpaka waombewe na mtoto wa Mungu mwingine. Huku ni kukosa ufahamu. Hakuna upendeleo kwa Mungu. Mtoto yeyote katika familia ya Mungu anakubaliwa na Baba aliye Mbinguni. Hakuna mtoto anayekubaliwa na Mungu zaidi anapoomba kuliko mwingine [SOMA MATENDO 10:34-35; WARUMI 2:10-11; KUMB.10:17]. Biblia inasema Mungu hapokei uso wa mwanadamu, yaani hamuoni mtoto wake mmoja kuwa ni bora kuliko wengine kiasi ya kwamba wengine asiwajali [WAGALATIA 2:6]. Eliya alipoomba mvua isinye kwa miaka 31/2; halafu akaomba tena mbingu zikatoa mvua; alikuwa katika hali ya mtoto wa Mungu kama yeyote yule. Alikuwa mwenye tabia moja na sisi, na Mungu hakufanya hayo kwa sababu aliomba Eliya! [YAKOBO 5:17-18].
Watu wengi waliookoka, wanatembea huko na huko katika mikutano wakihitaji kuombewa na watu wengine. Miongoni mwao, wako wanaofikiri sala ya mzungu fulani kutoka Marekani au Uingereza ndiyo ataisikia Mungu zaidi kuliko sala yake. Huku ni kukosa ufahamu. Mungu hapokei uso wa mwanadamu wala hana upendeleo. Kila aaminiye, akiomba hupokea. Ukifanya utafiti, utagundua kwamba, mara nyingi watu ambao wanapokea miujiza wanapoombewa na wengine; ni wale ambao hawajaokoka kabisa, au wale waliookoka lakini wakiwa na muda mfupi sana katika wokovu. Sababu ni kwamba, baada ya mtu kuwa na muda mrefu katika wokovu; unatazamiwa na Mungu kuchukua mwenyewe chakula na kukila bila kungoja kulishwa. Biblia inasema uponyaji ni chakula cha watoto wa Mungu [MATHAYO15:26]. Katika hali ya asili, mtoto anapozaliwa, katika uchanga hulishwa kwa kijiko na mtu mwingine, kwa sababu hawezi kujilisha mwenyewe. Mtoto huyo anapokua, anatazamiwa achukue kijiko na kula mwenyewe. Haitapendeza kumwona mtoto mwenye miaka kumi, akilishwa chakula na mtu mwingine. Vivyo hivyo katika maombi, kila mtu aliyeokoka anatazamiwa kuomba mwenyewe na kuchukua jibu lake. Kwa kukosa maarifa, watu wengi wa Mungu wameangamia [HOSEA 4:6]; na kukosa majibu ya maombi yao. Yafuatayo ni maarifa unayopaswa kuwa nayo ili upate majibu ya maombi yako kila mara.
A: MAMBO MANNE YA KUYAFAHAMU KABLA YA KUMWOMBA MUNGU LOLOTE
1. Mfahamu Vizuri Mungu Baba na Mungu Mwana
Kwa kuwa tunamwomba Mungu Baba kwa jina la Mungu Mwana-Yesu Kristo, ni vema sana kuwafahamu vizuri ili tuwe na hakika ya kujibiwa. Ufahamu ulio nao kuhusu mtu unayekwenda kumwomba hitaji lako, unaweza ukakupa imani ya kupokea kwake au ukakupunguzia imani hata ya kwenda kumweleza hitaji lako. Ukifahamu kwamba mtu fulani ni katili, ufahamu huo unatosha kuondoa ujasiri wa kumwomba lolote. Kwa kukosa kuwafahamu vizuri Mungu Baba na Mungu Mwana, watu wengi waliookoka wamekosa msingi mzuri wa kujibiwa maombi yao. Kinyume na inavyopasa, msingi wao wa kuomba unakuwa ni manung’uniko ambayo huleta maangamizo badala ya mafanikio [SOMA 1 WAKORINTHO 10:10]. Ukiwafahamu vizuri Mungu Baba na Mungu Mwana, ufahamu huo pekee, utakufanya uwe na hakika ya mambo unayotarajia kuyapata; ingawa hayajaonekana bado. Hii ndiyo inayoitwa IMANI ambayo ni msingi muhimu wa kupewa majibu yetu [WAEBRANIA 11:1,6]. Imani ni kuamini jinsi Neno la Mungu linavyoeleza kuhusu Mungu alivyo kwetu. Ukiwafahamu Mungu Baba na Mwana walivyo huwezi kunung’unika, kubabaika na kukata tamaa. Kunung’unika, Kubabaika na Kukata tamaa; ni kinyume kabisa na Imani. Watu wanaonung’unika, kubabaika na kukata tamaa, ni watu wasiomfahamu Mungu alivyo. Usiwe miongoni mwa watu wa jinsi hiyo, ambao hawawezi kupata majibu ya maombi yao.
Inakubidi basi, kuyafahamu yafuatayo na kuyaamini kabla ya kuomba; ili upate Majibu yaMaombi yako:
Mungu Baba hujishughulisha SANA na kila jambo tunalolihitaji, liwe dogo au kubwa. Wakati wote, fahamu kwamba hitaji ulilonalo anapenda kulishughulikia mno. Anataka tu, umtwike YEYE fadhaiko ulilo nalo. [SOMA 1 PETRO 5:6-7].
(b) Ni mapenzi ya Mungu Baba, kukupa haja za moyo wako na kukuona una furaha baada ya kujibiwa maombi [SOMA ZABURI 37:4; YOHANA 16:24].
(c) Mungu Baba anawahurumia watu waliookolewa kama vile Baba awahurumiavyo watoto wake [SOMA ZABURI 103:13]. Linalofurahisha zaidi ni kwamba, Mungu Baba; ni Baba mwenye uwezo wote, tofauti na baba wa duniani ambao wanaweza kuwa na huruma kwa watoto wao, lakini wakakosa uwezo wa kuwasaidia; wakabaki kusema “POLE”, bali huruma ya Mungu huambatana na UWEZO wa kutupa mahitaji yetu; hata yakiwa mazito kiasi gani. [ANGALIA MFANO LUKA 7:13-15].