Tuesday, December 24, 2013

ALIYETANGAZA MWISHO WA DUNIA AFARIKI


Mtu aliyeuchanganya ulimwengu kwa kutangaza tarehe ya mwisho wa dunia akaweka mabango katika kona mbalimbali za jiji la Dar es salaam, na kutoa matangazo kwenye vyombo vya habari Bw.Harold Camping, amefariki dunia.

Gazeti hili katika matoleo yake ya nyuma lilichapisha mkasa huo uliozua tafrani kubwa, wakati muda uliotarajiwa wa mwisho wa dunia ulipowadia bila ya tukio lolote kutokea, lakini baadae mtu huyo alijitia moyo na kurejea tena mbele ya wanahabari na kutoa ufafanuzi.

Kulingana na tangazo la wanafamilia wa Bw. Camping, alifariki dunia wiki iliyopita baada ya kuanguka nyumbani kwake, huku maelfu ya watu wakimiminika kushuhudia, huku wengi wakiwa hawaamini tangazo hilo la msiba.

Mwaka 2010, kituo cha Redio kinachomilikiwa na mtu huyo kilitangaza kuwa mwisho wa dunia ungekuwa mei 21, 2011. Kampeni kubwa ya kubandikwa kwa mabango duniani ikafanyika, ndipo mabango yenye utisho mkubwa yakaonekana katika maeneo ya Ubungo, Mwenge, Sinza na kwingineko.

Wanafamilia wamesema ndugu yao alifariki jumapili jioni akiwa na miaka 92. Mwajiliwa mmoja wa Radio ya Bw. Camping alithibitisha kutokea kwa kifo hicho na kuongeza kuwa amekuwa mdhaifu tangu mwaka 2011 alipopata shambulio la damu.

Inadaiwa kuwa kutotimia kwa unabii katika tangazo lake duniani kote kuwa dunia ingekwisha Oktoba 2011, baada ya kanisa kunyakuliwa Mei 2011, umemkera na kumpa msongo wa mawazo.

Mwaka 2011 haikuwa mara ya kwanza kutoa unabii feki, awali mwaka 1994 alikwisha kutabiri kuja kwa mwokozi kwa mara ya pili na hapo aliweza kuteka akili za watu na kuwafanya wengine wengi kuamini maneno yake kutokana na nguvu kubwa aliyokuwa akiitumia kueleza tabiri zake hizo.

Akiongea kwenye kituo chake cha radio, mwaka 2012 mara baada ya unabii wake kutotimia alisimama kuwa alikosea kutangaza tarehe hiyo kwani ilikuwa ina makosa katika kujumuisha tarakimu, akakiri kutenda dhambi na kuiacha huduma yake kando.

Mkanganyo huo ulimpelekea kuuza baadhi ya vifaa katika kituo chake cha radio na kuwaachisha kazi wafanya kazi wengi. Baadhi ya mitandao duniani ilimuelezea Bw. Camping kama nabii wa uongo, huku wengine wakumuelezea kuwa ni sehemu ya wale wanao papatikia kutoa nabii bila kuzithibitisha.

Wakala wake aliyekuwa akisambaza mabango ya mwisho wa dunia jijini Dar es salaam, Mbeya na kwingineko hakuwa tayari kuzungumzia tukio hilokwakuwa miongoni mwa nabii za mtu huyo ilikuwa ni kunyakuliwa hai na sio kufariki na kuzikwa kama wanadamu wengine. Mtu huyo amekuwa akimiliki kituo cha radio chenye kutangaza karibu dunia nzima tangu mwaka 1950.


CHANZO: GAZETI LA JIBU LA MAISHA(Toleo namba 273, jumapili desemba 22~28 2013)

No comments:

Post a Comment