Tuesday, December 3, 2013

KWANINI TUNAHUBIRI INJILI?



MUNGU akubariki rafiki popote ulipo na karibu katika somo hili ambalo tunajifunza kwamba ‘’KWANINI INJILI INAHUBIRIWA?

-Injili ni habari njema za ufalme wa MUNGU ambao umeletwa kwa wanadamu na BWANA YESU KRISTO .

-Injili ni mpango wa MUNGU wa kuwaokoa wanadamu kutoka mikononi mwa shetani.

Injili ni habari za uzima wa milele ambao unapatikana katika YESU KRISTO pekee(Yohana 14:6 , Matendo 4:12).

Mwanzo wa injili ndio mwanzo wa miaka pia maana kama mwaka huu ni 2013 basi maana ni miaka 2013 tangu BWANA YESU alete habari njema za ufalme wa MUNGU yaani INJILI.

Tukizungumzia injili tunazungumzia habari njema za za pekee za kwenda uzima wa milele. Na kama tutataka tuijue injili basi inapatikana pekee makanisani au kwenye semina za kiroho na kwenye mikutano ya injili na chanzo chke ni BIBLIA TAKATIFU na sio kwingine popote. Zile injili ambazo ziko nje na BIBLIA ni injili za uongo ambazo shetani ndio alizileta kupitia WAPINGA INJILI YA KWELI yaani WAPINGA KRISTO ambao wanamtumikia shetani na hawataki kuja kwenye nuru ya ulimwengu yaani kwa BWANA YESU.

ZIFUATAZO NI SABABU 4 ZA INJILI KUHUBIRIWA KATIKA ULIMWENGU WOTE.

1; KUTII AGIZO LA BWANA YESU.

Marko 16:15-16(Akawaambia, Enendeni ulimwenguni mwote, mkaihubiri Injili kwa kila kiumbe. Aaminiye na kubatizwa ataokoka; asiyeamini, atahukumiwa. ).

Mapenzi ya YESU ni kwamba tutoke na kuwaendea watu ili HABARI NJEMA iwafikie.

Warumi 10:13-14(kwa kuwa, Kila atakayeliitia Jina la BWANA ataokoka. Basi wamwiteje yeye wasiyemwamini? Tena wamwaminije yeye wasiyemsikia? Tena wamsikieje pasipo mhubiri? ).

Ndugu nimetumwa kwako na yeye na yeye anayejua maisha yako hadi mauti yako, ambaye anataka umpe yeye maisha yako ili awe BWANA na MWOKOZI wa maisha yako maana nje na yeye hakuna mwanadamu yeyote kupata uzima wa milele,(Yohana 14:6, Matendo 4:12). Hivyo kama tunataka uzima wa milele lazima tu tumfuate BWANA YESU na yeye yuko kwenye injili yake yaani kwenye BIBLIA.

2; MUNGU ANATHAMINI NAFSI YA MWANADAMU KULIKO VYOTE.

Yohana 3:16( Kwa maana jinsi hii MUNGU aliupenda ulimwengu, hata akamtoa Mwanawe pekee, ili kila mtu amwaminiye asipotee, bali awe na uzima wa milele. ).

Ndugu ulimwengu ni wewe hivyo MUNGU anataka uokolewe..

2 Kor 5:19 (yaani, MUNGU alikuwa ndani ya KRISTO, akiupatanisha ulimwengu na nafsi yake, asiwahesabie makosa yao; naye ametia ndani yetu neno la upatanisho. )

3; KUNA KUZIMU NA MATESO YA MILELE.

Ufunuo 20:11( Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana. ).

Injili inahubiriwa ili kwamba hata kama kuna mwanadamu ataenda kuzimu basi aende kwa kutaka yeye ila maonyo kutoka kwa MUNGU kupitia neno lake ambalo injili ni sehemu yake aliyapata.

Ndugu penda injili na penda kujiunga na watu wengine kanisani ili kujifunza na kulijua kusudi la MUNGU la uzima wa milele.

4; INJILI HULETA WOKOVU.

Warumi 1:16.(Kwa maana siionei haya Injili; kwa sababu ni uweza wa MUNGU uuletao wokovu, kwa kila aaminiye, kwa Myahudi(wa nyumbani kwako) kwanza, na kwa Myunani(watu wa nje) pia. )

Waebrania 2:3.(sisi je! Tutapataje kupona, tusipojali wokovu mkuu namna hii? Ambao kwanza ulinenwa na BWANA, kisha ukathibitika kwetu na wale waliosikia; )

-Ndugu Tafuta injili nawe utapona maana injili inaleta badiliko.

-Ingia kwa YESU na dhambi yako itakoma.

- Wokovu ni hatua ya kwanza na kuukulia wokovu ni hatua inayofuata hivyo mpendwa wangu penda kuhudhuria mafundisha kanisani.

-‘’KUMBUKA UKIPENDA IBAADA UTAKUWA UNAMPENDA MUNGU’’

MUNGU anakupenda sana ndugu ndio maana alimtuma BWANA YESU KRISTO ili wewe uwe na uzima sasa kisha uzima wa milele katika yeye.

- Ndugu injili ya kweli inaambatana na miujiza, uponyaji, kufunguliwa na kuwaweka watu huru kutoka kila pando la shetani, hivyo nenda kanisa ni utapona na pia utajifunza neno la MUNGU.

MUNGU akubariki sana na kama bado hujaokoka , ndugu chukua hatua hiyo leo na jina lako litaandikwa kwenye kitabu cha uzima, endelea na mafundisho na maombi na utamwona MUNGU kwa kila hatua ya maisha yako.

AMEN.

Ni mimi ndugu yako Peter Michael Mabula.

Maisha ya ushindi Ministry.

No comments:

Post a Comment