ILITOKEA lakini haikuandikwa kwa sababu haikudakwa!
Mchungaji wa Kanisa la Ufufuo na Uzima lenye makazi yake
kwenye Viwanja vya Tanganyika Perkas, Kawe jijini Dar,
Josephat Gwajima alinusurika kuuawa mara tatu kufuatia
kuvamiwa na majambazi watatu mwishoni mwa mwaka jana.
Akizungumza na Risasi Jumamosi hivi karibuni, Gwajima
alisema tukio hilo lilijiri nyumbani kwake, Mbezi Beach jijini
Dar ambapo siku ya kwanza, majambazi hao waliingia
nyumbani kwake saa nne usiku wakiwa wameficha sura na
kumkuta yeye sebuleni ambapo walimuuliza, ‘Gwajima yuko
wapi?’
“Ni kweli nilinusurika kifo na majambazi, walinivamia mara
tatu nyumbani. Zilikuwa siku mbaya maishani mwangu.
Siku ya kwanza walikuja na bunduki huku wameficha sura,
walinikuta sebuleni, wakaniuliza alipo Gwajima, niliwajibu
ametoka, wakaondoka wakisema watarudi kesho yake.
“Nilijua ni utani, lakini kweli siku iliyofuata saa nne usiku
walikuja tena, wakanikuta ndiyo naingia nyumbani,
wakaniambia niko chini ya ulinzi, nilimuomba Mungu aokoe
maisha yangu kwani nilipatwa na mshtuko, wakahoji;
‘Gwajuma yuko wapi?’ Kabla sijajibu mmoja akasema; ‘huyu
bwana mdogo ndiye tuliyemkuta jana,’ wakaondoka.
“Sikuwa na wazo la kuripoti polisi ila nilimwamini Mungu
aliye hai. Siku ya tatu walipitia juu ya paa kwa kung’oa vigae
na kushukia chumbani wakiwa na bunduki.
“Mimi nilikuwa kitandani na mke wangu, wakauliza tena
Gwajima yuko wapi? Nikawajibu bado hajarudi, wakasema;
‘haka (Gwajima) ndiyo kale kale ka bwana mdogo ka jana.’
“Mungu mkubwa, kwa nje zilisikika kelele za mbwa kisha
wakatoweka ghafla, niliona ni siku za majaribu kwangu,
nilimwomba Mungu atupilie mbali majaribu yale, baada ya
siku kadhaa niliamua kuhama kwenye nyumba ile.
“Ila nakumbuka ile siku ya mwisho walisema tunamtaka
Gwajima kwa sababu anajifanya kufufua misukule kisha
anataja majina yetu.
“Ndipo nilijua kumbe kisa ni kufufua misukule. Najua umbo
langu ndiyo mkombozi wa yote kwani waliponiona walijua
Gwajima hawezi kuwa na umbo dogo kama mimi nilivyo,”
alisema Gwajima.
Katika mahojiano marefu na gazeti hili, mchungaji huyo
alisema kuwa mpango wa kumuua uliofanywa na mtu
ambaye aliwahi kutajwa jina na binti msukule aliyemfufua
kanisani kwake. Alisema mtu huyo aliyetajwa na msukule
ni mtumishi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (jina
hakumtaja).
No comments:
Post a Comment