Saturday, January 4, 2014

Mchungaji auawa kwa risasi


WATU wanaosadikiwa kuwa ni majambazi wamemuua kwa kumpiga risasi
mchungaji wa Kanisa la Apostolic la mji mdogo wa Shirati,
wilayani Rorya, mkoani Mara.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalumu ya Tarime/Rorya,
Justus Kamugisha, licha ya kukiri kutokea kwa mauaji hayo, alisema hajui
kama aliyeuawa ni mchungaji na jeshi hilo linaendelea na
uchunguzi.
Habari zilizopatikana kutoka katika eneo la tukio zimemtaja Mchungaji
huyo kuwa ni Owiti Ariri.
Inadaiwa kuwa Mchungaji Ariri aliuawa muda mfupi baada ya
kukabidhiwa sanduku la fedha za kikundi cha kuweka na kukopa
alichokuwa akikifanyia kazi kama mhazini.
Kwa mujibu wa habari hizo zilizothibitishwa na Mchungaji Christopher Nyaitega, mara baada ya mauaji hayo, yaliyotokea Desemba 20 nyumbani kwa mchungaji huyo baada ya kuvamiwa na majambazi.
Habari zinasema kuwa mchungaji huyo alikabidhiwa fedha hizo Desemba 19 mwaka jana, majira ya alasiri katika moja ya hoteli iliyoko katika mji
huo.
Inaelezwa kuwa baada ya kukabidhiwa fedha hizo, mchungaji huyo alielekea nyumbani kwake akiwa na sanduku hilo lililokuwa limejaa fedha.
Mchungaji Nyaitega ambaye hata hivyo hakuweza kujua kiasi cha fedha
kilichokuwemo ndani ya sanduku hilo, alisema wana kikundi waliamua kumkabidhi fedha hizo ili
aziwahishe benki kesho yake.
Alisema akiwa nyumbani kwake, majira ya jioni alitembelewa na mmoja
wa wana kikundi na kuanza kudadisi kuhusu fedha hizo na marehemu alimhakikishia kuwa ziko salama.
Mchungaji Nyaitega alisema muda mfupi baada ya mwana kikundi huyo kuondoka,
ghafla majambazi walifika nyumbani hapo na kumtaka marehemu awape
fedha hizo kabla ya kumuua kwa kumpiga risasi.
CHANZO: GAZETI LA TANZANIA DAIMA

No comments:

Post a Comment