MWIMBAJI chipukizi wa nyimbo za injili, Upendo Mollel amewaasa waimbaji wenzake nchini kujitafakari na kujipima kuwa mwaka huu watamtumikia Mungu kwa viwango gani.
Akizungumza na Tanzania Daima katika mahojianio maalumu, Mollel alisema ni vyema waimbaji wa nyimbo za injili wakajitambua kuwa ni watumishi wa Mungu na wanapeleka neno lake kwa kasi zaidi kuliko muhubiri yeyote.
Mollel ambaye kitaaluma ni mwalimu, alisema kuwa nyimbo za injili zisichukuliwe sehemu ya biashara kama baadhi ya waimbaji wengine wanavyofanya, bali iwe ni sehemu ya huduma kamili ya kiroho.
“Najua kuandaa albamu mpaka iweze kuwafikia wasikilizaji au iingie sokoni ni gharama kubwa, lakini imefikia hatua waimbaji sasa wameondoka katika mlengo wa huduma na sasa wamekaa kibiashara zaidi, inasikitisha mwimbaji anapopewa mwaliko anaanza kutaja gharama kubwa ambazo wakati mwingine yule anayemwalika anashindwa kuzimudu.
“Hii ni kazi ya Mungu kabisa, hivyo isifikie hatua waimbaji wakageuza kuwa ni biashara, kumbuka uimbaji ni karama tu na Mungu akiamua anaweza kukunyang’anya karama hiyo na kumpa mtu mwingine, wapo watumishi wengi wanalalamika kuwa kwa sasa kumwita mwimbaji kuja katika huduma ya mkutano ni gharama kubwa jambo ambalo mimi kimsingi linaniumiza sana,” alisema.
Mollel ambaye kwa sasa yupo mbioni kuzindua albamu yake ya video, alisema kuwa pia anatamani sana waimbaji wa nyimbo za injili nchini wangeunda umoja wao na kufungua studio yao ili kurahisisha kazi ya Mungu kusonga mbele.
“Natamani sana kusikia kuna umoja wa waimbaji wa muziki wa injili na kama wangeweza kujenga hata studio kubwa kwa ajili ya kufanya shughuli hiyo, jambo hilo lingesaidia hata waimbaji chipukizi kama sisi ili tuweze kufanya kazi ya Mungu bila wasiwasi, pia wapo waimbaji wengi huko vijijini nao wangetiwa moyo na vipaji vyao vingeonekana na wangemkomboa mwanadamu kutoka katika utumwa wa dhambi,” alisisitiza.
Mwimbaji huyo aliongeza kuwa kwa sasa anafanya matayarisho ya kukamilisha albamu yake hiyo itakayokuwa na nyimbo nane ikijulikana kwa jina la ‘Sijaona Kama Wewe Mungu’.
No comments:
Post a Comment