Saturday, October 26, 2013

T.A.G KUREJESHA MAADILI




UKOSEFU wa maadili katika jamii madhara yake ni makubwa.

Watu wengi wamekuwa wakilizungumza hilo, lengo likiwa ni kuwashawishi wazazi na walezi wawalee vijana wao katika misingi mema.

Kwa kuliona hilo Kanisa la Tanzania Assemblies of God (TAG) chini ya Kiongozi Mkuu Mchungaji Dunstan Kanemba limezindua mkakati wa kugeuza mioyo ya watu kwa kueneza Neno la Mungu.

Mkakati huo umefanikiwa ambapo mateja, vibaka, majambazi na mashoga wameamua kubadili tabia zao na kuwa watu wema katika jamii.

Mchungaji Kanemba anasema Magomeni inajulikana ni miongoni mwa maeneo yenye vitendo vya ukosefu wa maadili ambapo biashara za dawa za kulevya, changudoa kuwaibia wanaume wasiowafahamu kwa kutumia mfumo wa kuwawekea dawa za kulevya kwenye vinywaji vyao na kuwaibia kila kitu vimashamiri.

Kwa kuliona hilo, Mchungaji Kanemba amezindua mkakati wa muda mfupi (miezi minne) ili aweze kuwafikia watu kwa injili ya upendo chini ya kaulimbiu ya “Ushuhudiaji wenye shabaha.”

Mkakati huo ulizinduliwa Agosti 4 mwaka huu.

Lengo ni kuwafikia Watanzania bila ubaguzi kwa kuwashirikishia habari njema za upendo wa Mungu.

Anasema kupitia mkakati huo rushwa haitakuwepo, magereza yatakosa wafungwa na uchumi utakua.

“Yanayotokea kama ufisadi, masuala ya rushwa ni matokeo ya jamii kukosa maadili na uzalendo kwa ujumla wake kwani ni aibu kwa Mtanzania yeyote kuomba rushwa kwani ni ukosefu wa maadili uliopitiliza.

“Ukienda nchi zilizoendelea kama Marekani huwezi ukakuta Mmarekani anamuomba rushwa Mmarekani mwenzake,” anasema.

Akieleza mkakati wa kurejesha maadili Mchungaji Kanemba anasema wameanzia katika Tarafa ya Magomeni yenye kata sita za Mzimuni, Magomeni, Ndugumbi, Kigogo, Mburahati na Makurumla.

Tangu mkakati kuzinduliwa, anasema tayari wameshafikia vitongoji vinne ambavyo ni Mzimuni, Magomeni, Ndugumbi na Kigogo.

Anasema njia ambazo wamekuwa wakizitumia ni ushuhudiaji wa mtu mmoja mmoja na mikutano midogo midogo ya mihadhara.

Njia nyingine ni kupitia matangazo kwa kutumia vyombo vya habari na mfumo wa kuonyesha filamu zenye ujumbe wa neno la Mungu.

Anasema mpango huo wa ushuhudiaji wenye shabaha utakuwa wa muda mrefu kwani hawana mpango wa kuishia Magomeni tu bali kufika maeneo mengine.

Akielezea matokeo ambayo wameyapata tangu kampeni hiyo izinduliwe, Mchungaji Kanemba anasema watu bila kujali utofauti wa imani zao wameupokea mkakati vizuri sana.

Kwa sasa anasema vibaka, mateja, mashoga, wachawi na watu waliokuwa wamekata tamaa wengi wamebadili tabia zao na kuamua kumfuata Mungu kiasi kwamba hata kanisa analoliongoza limekuwa dogo kutokana na mwitikio mkubwa.

“Nitumie fursa hii kuwashukuru wananchi wa Magomeni kwa kuupokea mkakati wa ushuhudiaji wenye shabaha, huku tukiunga mkono kampeni ya Mkuu wa Jeshi la Polisi, IGP Said Mwema ya ‘Utii wa Sheria Bila Shuruti’, hivyo kampeni hii ina msaada mkubwa kwa polisi.

“Sisi kama kanisa kazi tunayoifanya ni kubadilisha mioyo ya watu ili waweze kuwa raia wema wanaotii sheria bila shuruti.

“Ndugu mwandishi, hata mimi sikutegemea kama mkakati huu unaweza kuwa na mafanikio kiasi hiki, maana watu ambao tumewafikia ni wale ambao kwa dhati walikuwa kero kwa jamii kutokana na tabia zao kuwa mbaya. Leo hii wamebadilika na wako kanisani wakiendelea kulelewa vyema kiroho.

“Leo hii kuna wanaume waliokuwa mashoga wamebadili tabia na kutangaza hadharani kuwa sasa wameokoka…kwa kweli hata mimi napenda kumshukuru Mungu sana. Kutokana na mwitikio huo imefikia hatua hata IGP kupitia kamanda wake wa Kinondoni ameweza kututia moyo na kuupongeza mkakati huu. Kwa dhati umeweza kuwafikia walengwa waliokuwa wameshindikana kwenye jamii,” anasema.

Anasema wana mpango wa kuwafikia hata vigogo kwa njia ya mikutano, magazeti, redio na runinga ili nao waweze kubadili tabia kwani suala la maadili mema ni la watu wote bila kujali hadhi ya mtu.

Akieleza changamoto zinazowakabili, Mchungaji Kanemba anasema kiukweli watu wameupokea mkakati wao, lakini tatizo linalowakabili ni namna ya kuwawezesha wale ambao wameamua kubadili tabia zao.

Mfano kuna watu walikuwa majambazi, changudoa na mashoga, hivyo anaiomba jamii, serikali na kampuni kuwasaidia fedha ili waweze kuwawezesha watu hao waliobadili tabia zao.

SOURCE: TANZANIA DAIMA 26/10/2013

No comments:

Post a Comment